Tuesday, 7 April 2015

POLENI MLIOACHWA, MLIOPIGWA NA KUNUNIWA PASAKA

Asante Mungu, muumba wa mbingu na ardhi kwa kuwa nimeiona Sikukuu ya Pasaka na leo ni Jumanne bado naendelea kuvuta pumzi yako, sifa na utukufu zikufikie.Wapenzi wasomaji wa safu hii napenda kuwakaribisha kwa mara nyingine tena kwenye mada yetu ya leo. Kwani ni wazi kuwa watu walio kwenye uhusiano wa kimapenzi watakuwa wameachwa, wamepigwa, wametengwa au wamenuniwa wakati wa sikukuu hii ya Pasaka.
Kwa imani ya Kikristo kuanzia Alhamisi Kuu mpaka Jumapili (Siku ya Pasaka yenyewe) ni siku za kuazimisha mateso, kifo, ufufuko na utukufu wake Yesu Kristo.Lakini kidunia watu wengine wanaigeuza siku hii kuwa ya kufanya ufuska na kila aina ya uovu kwa sababu tu wengi wao wanakuwa na uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kula na kunywa chochote wakipendacho.
Tumeshuhudia vyombo mbalimbali vya habari vikitangaza na kuonyesha matukio ya mafumanizi katika kipindi hicho cha Pasaka, bila shaka kwa matukio hayo ni wengi sana watakuwa wameachana au kutengana na wapenzi wao.
Wapo wengine waliojifunza kunywa kilevi katika siku hii, wengine kuvuta sigara, kutumia dawa za kulevya. Si ajabu kuona ama kusikia wapendanao wakiwa wamegombana kwa sababu mwenzi wake katumiwa kadi ama salamu za Pasaka, na ugomvi unakuja pale mwenza anapoamua kupiga namba iliyotuma salamu hizo na kubaini ni jinsia tofauti na mwenzi wake kisha kuanza kulumbana kabla ya kugombana.
Pole sana kama umenuniwa kwa sababu tu hukutimiza majukumu kwa mwenzi wako, kama vile kumnunulia nguo, viatu, chakula, vinywaji kumtoa out na mengineyo. Kama ulifanya hivyo makusudi kwa sababu humpendi au una mpenzi mwingine, ni jambo unalolijua mwenyewe.
Najua kuna wengine wameumizwa na wapenzi wao kwa sababu hawakuwa na fedha za kuwapeleka kubarizi kwenye fukwe kisha kuamua kutoroka kwa kwenda na michepuko yao.Kama wewe ni mmoja wa wale walioachwa kwa kosa la kushobokea mastaa waliokuwa wanafanya shoo katika majumba mbalimbali ya starehe zilizofanyika siku ya Pasaka, pole sana.
Bila kuwasahau mliojikuta mkijiingia kwenye uhusiano mpya wa kimapenzi pasipo kuwachunguza wapenzi wenu wapya, naamini baadaye wapo watakaojilaumu na wengine kufurahia uhusiano huo.Ninaamini kuna wengine wameaibika na kutembezewa kichapo cha nguvu, kiasi cha kunusurika kifo au kufa kabisa baada ya kufumaniwa na mpenzi wa mtu.
Sherehe za kidini ni kumbusho la waamini husika kufuata yale wanayopaswa kufanya katika kuonyesha utukufu wa viongozi wao wa kiimani na kutukuza utukufu wa Mwenyezi Mungu na siyo siku ya kufanya maovu.
Huu mwisho wa makala hii, tuungane wiki ijayo katika makala nyingine.

POLENI MLIOACHWA, MLIOPIGWA NA KUNUNIWA PASAKA Rating: 4.5 Diposkan Oleh: Boss Ngasa

0 comments:

Post a Comment

LinkWithin