Friday, 13 March 2015

BAADA YA KUTAKA AUAWE KWA KUKOSA MTOTO MCHUNGAJI AMWITA JIDE AMUOMBEE!


Imelda Mtema/Ijumaa
SIKU moja tu baada ya mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Jide’ kutupia kwenye mtandao wa Instagram, Jumanne iliyopita akisema baadhi ya watu wanamsakama kuhusu kutozaa bora auawe, mchungaji ameibuka na kumtaka staa huyo kufika kanisani kwake ili amwombee.
Mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Jide’.
Mchungaji Overcomer Daniel wa Kanisa la Mlima wa Makimbilio, Boko, Dar es Salaam ndiye aliyemtaka staa huyo akisema tatizo lake la kutopata mtoto analijua kwa vile linawakabili wanawake wengi kwa sasa.
JIDE aliandika hivi
Hivi watu hamuelewi Kiswahili au ni nini??? Nimesema tumbo limevimba sababu ya sahani, nikimaanisha mlo na niliposti nakula hapo awali.Sasa hapo maneno mengine yanatokea wapi? Au niwe naandika Kichina? Kwani mliambiwa nitazaa rais atakayewatoa kwenye shida zote mpaka mnishikilie mimba mimba...Hebu niacheni basi, khaa! Nisiishi kisa mimba? Basi niueni kisa sizai....
KOANZIA
Baada ya kupata ujumbe wa Jide kupitia mtandao huo huku pia akiwa ameshasoma habari zake muda mrefu kuhusu kutopata mtoto kwenye ndoa yake, Mchungaji Overcomer alipiga simu chumba cha habari cha Magazeti Pendwa ya Global Publishers na kuongea na Mhariri Kiongozi wa magazeti hayo, Oscar Ndauka.
Baada ya salamu, akasema: “Mimi ni Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Makimbilio, lipo Boko. Aaa! Naitwa Overcomer Daniel. Nina ibada ya kuwaombea watu mbalimbali wenye mahitaji ambayo kwao ni mlima.
“Sasa nimeona mwanamuziki Lady Jaydee anazungumzia suala la kukosa mtoto. Hapa kwetu Mungu anatenda. Si kwa Jide tu, kwa mtu yeyote, awe mwanamuziki, mcheza mpira, mama wa nyumbani, baba wa kawaida, mwanafunzi, yaani mtu yeyote yule, namkaribisha kuja kumwombea kwa matatizo aliyonayo.
“Naamini watabarikiwa na matatizo yao yatapata ufumbuzi kwa muujiza wa Mungu aliye hai,” alisema mchungaji huyo.

WANAWAKE KUKOSA KUZAA
Mchungaji huyo alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, wanawake kukosa kushika mimba si suala la miaka hii. Tangu zamani zile, ilikuwa hivyo.“Mfano, mke wa Ibrahim (Abrahamu), Sara (Sarai) naye alikuwa hashiki ujauzito tangu ameolewa. Lakini akiwa na umri wa miaka karibia themanini, Mungu alimwonesha kwamba hata katika umri huo, mwanamke anaweza kutendewa muujiza akapata mtoto (Mwanzo 21:1-2).
Aliyekuwa mume wa Judith Wambura Mbibo ‘Jide’ Gardner G. Habash.
“Sara alipata ujauzito akamzaa Isaka. Sasa baadhi ya binadamu wa leo wanapokuwa katika hali hiyo wanakata tamaa mapema. Ndiyo maana nawaita wote wenye shida hiyo na nyingine waje Mlima wa Makimbilio,” alisema Mchungaji Overcomer.
IJUMAA LAMSAKA JIDE
Baada ya ujumbe wa mchungaji huyo, Ijumaa lilimtuma paparazi wake kumtafuta Jide ili kumpa mwaliko huo.Jide hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi baada ya namba zake kuwa za tabu kupatikana. Hata hivyo, Ijumaa lilifika nyumbani kwake, Kimara Temboni, Dar ambako hivi karibuni ilidaiwa amerudi kuishi hapo.
NYUMBA YA JIDE TUPU
Ijumaa liliikuta nyumba hiyo ikiwa na dalili zote za kutoishi watu kutokana na mazingira ya nje. Baadhi ya majirani walisema hakuna binadamu yeyote anayeishi ndani ya nyumba hiyo kwa sasa.
“Jide hakai hapa. Siku nyingi hatujamuona. Lakini pia mnavyoona kwa nje, nyumba hii hakai mtu. Kuhusu hiyo namba yake, sisi majirani hatuna,” alisema jirani mmoja aliyekataa kujitambulisha kwa jina.
IJUMAA LAMSAKA GARDNER
Baada ya kutoka Kimara, Ijumaa lilimsaka ‘mtalaka’  wa Jide, Gardner G. Habash ambapo mazungumzo yake na gazeti hili yalikuwa hivi:
Ijumaa: “Habari za kazi?”
Gardner: “Njema.”
Ijumaa: “Samahani sana, nawezaje kupata namba za simu za Jide?”
Gardner: “Mh! Kwa kweli siwezi kukupatia kwa sababu mwenyewe hataki kabisa. Sasa kwa sababu hataki, kukupa namba yake ni sawa na kumsaliti.”   

BAADA YA KUTAKA AUAWE KWA KUKOSA MTOTO MCHUNGAJI AMWITA JIDE AMUOMBEE! Rating: 4.5 Diposkan Oleh: Boss Ngasa

0 comments:

Post a Comment

LinkWithin