Monday, 16 March 2015

ANA UJAUZITO WAKO? MSAIDIE KWA KUFANYA HAYA-2Ni wiki nyingine tunapokutana tena kwenye ukurasa wetu huu mzuri, tukijuzana na kuelimishana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Wiki iliyopita tulianza kuijadili mada ya nini cha kufanya ili kumsaidia mwenzi wako anapokuwa na ujauzito.
Nakushukuru wewe msomaji wangu ambaye ulishiriki kutuma ujumbe wako na kutoa ushauri kwa msomaji Jackson wa Morogoro ambaye alikuwa akilalamika jinsi mkewe alivyobadilika tabia baada ya kubeba ujauzito kiasi cha kuwa anamkasirisha mara kwa mara.
NI HALI YA KAWAIDA
Wasomaji wangu wengi, hasa ambao tayari wanao uzoefu wa mabadiliko yanayotokea katika kipindi cha ujauzito, wamesema kwamba ni jambo la kawaida kabisa kwa mwanamke kubadilika kitabia na kihisia baada ya kunasa ujauzito.
“Mimi mwenyewe wakati nikiwa mjamzito, nilikuwa namchukia sana mume wangu kiasi cha kuwa nalala sebuleni kila siku ili kukwepa kulala naye. Nilikuwa naona ananikera kila kitu anachokifanya lakini namshukuru mume wangu alinielewa. Nilipojifungua, kile kisirani kimeisha kabisa na tunapendana sana,” alichangia msomaji wangu, Mama Kelvin wa Tabata.
Jambo muhimu la kujifunza, ni kwamba mwenzi wako anapobadilika tabia kwa sababu ya ujauzito, elewa kwamba hiyo ni hali ya kawaida kabisa na itaisha baada ya muda mfupi, cha msingi ni kumvumilia na kuendelea kumuonesha mapenzi ya dhati.
NAMNA YA KUISHI NA MWENZI MJAMZITO
Hakuna kipindi ambacho mwanamke anahitaji kuoneshwa kwamba unampenda, unamjali na unafurahia yeye kuwa na mzigo wako kama kipindi ambacho anakuwa na ujauzito.
Jambo ambalo watu wengi hawalijui, baada ya ujauzito kufikia kipindi fulani, mtoto anayekuwa tumboni anachangia vitu vingi sana na mama yake. Mama anapokasirika, anazalisha kemikali/homoni ambazo zinaenda kumuathiri mtoto moja kwa moja tumboni.
Hali kadhalika, mama akiwa anafurahi mara kwa mara, mtoto aliyepo tumboni naye anafurahi na hata ukuaji wake unakuwa mzuri. Hata kama hukuwa na mazoea ya kuwa karibu na mwenzi wako awali, jifunze kuwa karibu naye, kumbembeleza, kupiga naye stori za kufurahisha na kumueleza jinsi unavyofurahi kuelekea kuitwa baba wa mtoto aliye ndani ya tumbo lake.
Mbusu tumbo lake mara kwa mara, msikilize mtoto anavyocheza na msaidie kufanya mazoezi mepesi ikiwa ni pamoja na kutembea pamoja jioni, kuhakikisha anapata chakula bora na matumizi mengine muhimu na kubwa zaidi muandalie mazingira salama ya kujifungulia.
Hivi ni vitu ambavyo vitamjenga sana mwenzi wako kisaikolojia na hakika vitamsaidia hata kuja kujifungua salama.
Epuka kumkaripia, kumuudhi au kumpiga mwenzi wako akiwa mjamzito.
  Msamehe kwa kila anachokosea, jirekebishe kwa kila kinachomuudhi na mara zote muonee huruma kwani kuna kazi kubwa inakuja mbele yake, ya kukuletea mtoto duniani.
Ukifanya hivyo, hakika utakuwa mwanaume bora na baba bora wa familia.

ANA UJAUZITO WAKO? MSAIDIE KWA KUFANYA HAYA-2 Rating: 4.5 Diposkan Oleh: Boss Ngasa

0 comments:

Post a Comment

LinkWithin